
Utangulizi
Migogoro ya ardhi ni miongoni mwa migogoro inayojitokeza mara nyingi nchini Tanzania. Chanzo chake kinaweza kuwa ni mipaka ya ardhi, umiliki wa kiwanja au shamba, urithi wa ardhi, uvamizi wa ardhi, upangishaji, matumizi ya ardhi, pamoja na madai ya fidia. Ili kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka na kwa gharama nafuu, Tanzania imeanzisha mfumo maalumu wa utatuzi wa migogoro ya ardhi unaosimamiwa na The Land Disputes Courts Act, Sura ya 216 (zamani Sheria Na. 2 ya mwaka 2002) pamoja na sheria nyingine za ardhi. Mfumo huu unaweka utaratibu wa kuanzia ngazi ya kijiji hadi Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Sheria Zinazosimamia Migogoro ya Ardhi
Migogoro ya ardhi husimamiwa hasa na sheria zifuatazo:
1. The Land Disputes Courts Act, Cap. 216 โ inayoweka mfumo wa mahakama za ardhi na mamlaka yake.
2. The Land Act, Cap. 113 โ inayosimamia masuala ya ardhi ya jumla.
3. The Village Land Act, Cap. 114 โ inayosimamia ardhi za vijiji.
4. The Ward Tribunals Act, Cap. 206 โ kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya kata katika maeneo yanayohusika.
Hatua za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
Hatua ya Kwanza: Baraza la Ardhi la Kijiji (Village Land Council)
Kwa migogoro inayotokea ndani ya kijiji, mlalamikaji huanza katika Baraza la Ardhi la Kijiji.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 7 cha Land Disputes Courts Act, Baraza la Ardhi la Kijiji lina jukumu la kufanya usuluhishi (mediation) badala ya kutoa hukumu. Madhumuni yake ni kuwafanya wahusika wafikie makubaliano ya hiari.
Aidha, Kifungu cha 8 kinaeleza utaratibu wa usuluhishi, na iwapo usuluhishi utashindikana, Kifungu cha 9 kinaelekeza kuwa shauri lihamishiwe Baraza la Ardhi Kata kwa utaratibu kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 62 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji.
Hatua ya Pili: Baraza la Kata (Ward Tribunal)
Iwapo usuluhishi wa kijiji hautafanikiwa, shauri hupelekwa Baraza la Kata.
Baraza hili limeanzishwa kwa kila kata kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha The Land Disputes Courts Act, na lina mamlaka ya kusikiliza na kupatanisha pande mbili zenye mgogoro ili zifikie makubaliano kwa ridhaa yao. Ni muhimu kutambua kwamba hapo zamani mabaraza haya ya kata yalikuwa na uwezo wa kufanya uamuzi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria mabaraza haya yanapaswa kusuluhisha tu na pale usuluhishi unaposhindana, baraza linapaswa kutoa cheti cha kushindwa kusuluhisha ili kuruhusu mgogoro kupelekwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya hii ni kwa Mujibu wa kifungu cha 13 cha Land Disputes Courts Act.
Katika hatua hii, pande zote zinaweza kuwakilisha vielelezo kama:
– Barua za manunuzi.
– Barua za serikali.
– Ramani.
– Ushahidi wa mashahidi.
– Picha au vielelezo vingine vinavyohusu umiliki au matumizi ya ardhi.
Hatua ya Tatu: Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya (District Land and Housing Tribunal)
Iwapo usuluhishi umeshindikana katika baraza la kata, na likatoa Cheti cha kushindwa kusuluhisha kwa upande ambao haujaridhika na usuluhishi basi mgogoro huo utapelekwa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
Baraza hili lina mamlaka makubwa zaidi ya:
– Kusikiliza mashauri mapya yaliyo ndani ya mamlaka yake.
– Kusikiliza rufaa kutoka Baraza la Kata.
– Kutoa amri mbalimbali kuhusu umiliki, matumizi na umiliki halali wa ardhi.
Baraza a hili inaongozwa na Mwenyekiti mwenye sifa za kisheria na hutumia pia washauri (assessors), katika kutoa maamuzi yake Mwenyekiti atazingatia ushauri wa washauri(assessors) ingawa halazimishwi kuufuata, hata hivyo asipoufuata sheria inamtaka kueleza sababu za kutofuata ushauri huo katika maamuzi yake. Baraza hili lina sura kamili ya mahakama na hufanya maamuzi kuhusu umiliki.
Ikumbukwe ingawa ni takwa la kisheria kwa kesi yoyote kabla ya kupelekwa kwenye baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya, kuwa na Cheti cha kushindwa kusuluhisha, yapo mazingira ambayo mlalamikaji ambaye hajaridhika anaweza kupeleka kesi bila kuwa na Cheti cha kushindwa kusuluhisha kutoka Baraza la Kata.
Hatua ya Nne: Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Ardhi)
Mtu asiporidhika na uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya anaweza kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Divisheni ya Ardhi.
Mahakama Kuu hupitia:
– Uhalali wa matumizi ya sheria.
– Tathmini ya ushahidi.
– Uhalali wa maamuzi yaliyotolewa na mahakama za chini.
Mahakama inaweza kuthibitisha, kubadilisha au kufuta uamuzi uliotolewa.
Hatua ya Tano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania
Hii ndiyo ngazi ya mwisho katika mfumo wa kawaida wa rufaa za migogoro ya ardhi.
Mahakama ya Rufani husikiliza rufaa zinazotokana na Mahakama Kuu kuhusu masuala ya sheria kwa mujibu wa taratibu zinazotumika.
Uamuzi wake huwa wa mwisho isipokuwa pale sheria inapoweka utaratibu mwingine maalumu.
Mlolongo wa Mahakama za Migogoro ya Ardhi
Mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini Tanzania ni:
1. Baraza la Ardhi la Kijiji.
2. Baraza la Ardhi Kata.
3. Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
4. Mahakama Kuu ya Tanzania (Land Division).
5. Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Mlolongo huu umeainishwa na Kifungu cha 3(2) cha Land Disputes Courts Act, kinachotambua mahakama zenye mamlaka ya kushughulikia migogoro ya ardhi.
Je, Unaweza Kuruka Hatua?
Kwa kawaida, Hapana.
Sheria inataka mgogoro uanzie kwenye chombo chenye mamlaka kwa eneo husika. Endapo shauri litafikishwa moja kwa moja kwenye mahakama isiyo na mamlaka ya awali, linaweza kutupiliwa mbali kwa sababu ya kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria. Hata hivyo, kuna mazingira maalumu yaliyowekwa na sheria ambapo shauri linaweza kuanzishwa moja kwa moja katika mahakama yenye mamlaka, kutegemeana na aina ya ardhi au mgogoro husika.
Umuhimu wa Ushahidi
Katika migogoro ya ardhi, ushahidi ndio msingi wa mafanikio ya shauri. Miongoni mwa ushahidi muhimu ni:
– Hati ya Umiliki (Certificate of Title).
– Offer Letter (Barua ya Toleo).
– Barua za Serikali.
– Mikataba ya mauziano.
– Ramani za upimaji.
– Ushahidi wa mashahidi.
– Picha za eneo.
– Taarifa za wataalamu wa upimaji.
Hitimisho
Mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini Tanzania umeundwa ili kuhakikisha migogoro inatatuliwa hatua kwa hatua kwa kuanzia usuluhishi katika ngazi ya jamii kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za juu. Ni muhimu kwa kila mwananchi kufahamu chombo chenye mamlaka ya kusikiliza mgogoro wake na kufuata utaratibu uliowekwa na sheria. Kufanya hivyo huongeza uwezekano wa kupata haki kwa wakati na hupunguza gharama na ucheleweshaji wa mashauri.
Discover more from ๐๐๐๐๐๐๐๐๐๐โ๏ธ
Subscribe to get the latest posts sent to your email.

