(De facto union)
Bila shaka itakuwa si jambo geni sana masikioni mwa wengi, jambo la watu ambao huishi kama mke na Mume pasipo ndoa rasmi, ama kwa lugha ya mtaani hujulikana kama sogea tukae. Katika sheria ya Tanzania, dhana ya Presumption of Marriage inamaanisha kwamba mahakama inaweza kutambua uwepo wa ndoa hata kama haikusajiliwa rasmi, ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa wahusika waliishi kama mume na mke kwa muda mrefu. Hii inatokana na Kifungu cha 160 cha Sheria ya Ndoa ya Tanzania, Sura ya 29.
Kanuni ya msingi ni kwamba pale ambapo hakuna Cheti cha Ndoa au Sherehe ya ndoa kwa namna yoyote iwe kidini, kimila au kiserikali basi HAKUNA NDOA. Dhana hii ya Ndoa inachukuliwa kama mahusiano tu ya watu wanaoishi katika nyumba moja na chini ya paa moja (cohabiting couples) kama mume na mke bila kuwa na ndoa rasmi iliyosajiliwa. Kwa hiyo watu hawa huishi chini ya udhani wa Ndoa.
Dhana ya udhani wa ndoa chini ya Common law, inachukuliwa kama kushindwa kufuatwa taratibu za kisheria za ndoa halali. Na ndio maana dhana hii pia hujulikana kama Common Law marriage.
Ili kuwe na dhana hii ya Ndoa yaani presumption of marriage, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
1. Muda wa kuishi pamoja
Wahusika wanapaswa kuwa wameishi pamoja kwa kipindi kirefu kwa namna inayoonyesha mahusiano kama ya ndoa. Hakuna muda maalum ulioainishwa kisheria, lakini mahakama huangalia hali halisi ya maisha yao.
2. Maisha kama ya ndoa (Cohabitation as Husband and Wife)
Wanandoa hao wanapaswa kuwa wameishi kama mke na mume mbele ya jamii zao, ndugu na marafiki. Wanaweza kuwa na watoto pamoja au kushiriki majukumu ya kifamilia kama wanandoa.
3. Utambulisho kwa jamii
Ikiwa jamii inayowazunguka inawatambua na kuwaona kama wanandoa, hili linaweza kusaidia kuthibitisha ndoa kwa dhana ya presumption of marriage. Ushahidi wa sherehe ya kimila au desturi fulani inayothibitisha ndoa pia unaweza kuzingatiwa.
4. Matumizi ya mali kwa pamoja
Ikiwa wanashirikiana katika masuala ya kifamilia kama vile kununua mali, kumiliki akaunti za benki kwa pamoja, au kushirikiana katika majukumu ya kifamilia, hili linaweza kusaidia kuthibitisha ndoa kwa dhana hii.
5. Kutokuwepo kwa ndoa nyingine halali
Ikiwa mmoja wa wahusika alikuwa tayari ameoa/kuolewa na ndoa hiyo bado haijavunjwa, basi presumption of marriage haiwezi kutambuliwa kwa sababu haiwezi kuwepo ndoa mbili kwa mtu mmoja kisheria (isipokuwa ndoa ya Kiislamu au ya kimila ambayo inaruhusu wake wengi).
KWANINI KUWE NA DHANA HII YA NDOA KWA UDHANI(PRESUMPTION OF MARRIAGE).
Kwa mtazamo wa jumla dhana ya ndoa ya udhani ilianzishwa kwa lengo la kuwalinda, wale wanaoishi kama mume na mke pasina ndoa halali na watoto wao, dhidi ya madhara yanayoweza kutokea endapo mmoja kati yao atakataa kwamba hakuwa akiishi na mwenzake kama mke na mume. Hata hivyo zifuatazo ni sababu nyingine za kuwepo kwa dhana hii
1. Kulinda haki za wake wa mitala na wake wa ndoa za kimila β Katika baadhi ya jamii, watu huishi kama wanandoa kwa muda mrefu bila ndoa rasmi, hasa katika ndoa za kimila au mitala. Presumption of Marriage inasaidia kutambua na kulinda haki za wake katika ndoa kama hizo.
2. Kulinda maslahi ya wanawake na watoto β Wanawake wengi wamekuwa wakitelekezwa na wenzi wao baada ya kuishi nao kwa muda mrefu bila ndoa rasmi. Dhana hii inahakikisha kuwa wanawake na watoto wanapata haki zao, kama vile matunzo na urithi.
3. Kuzuia udanganyifu wa ndoa β Watu wengine hujitahidi kukwepa majukumu ya ndoa kwa kudai kuwa hawajawahi kufunga ndoa, hata kama wameishi na mwenza wao kwa muda mrefu. Dhana hii inalinda haki za mwenza aliyeathirika kwa kuthibitisha uwepo wa ndoa kwa kuzingatia mwenendo wa maisha yao.
4. Kulingana na misingi ya haki na usawa β Sheria nyingi zinajaribu kuhakikisha haki sawa kwa wote, hasa pale ambapo mwanamke au watoto wanaweza kuathirika kutokana na kutokuwepo kwa ndoa rasmi.
Ni muhimu kukumbuka kuwa ili dhana ya ndoa ya udhani, iwepo ni lazima mwanaume na mwanamke wanaoishi kama mume na mke pasipo ndoa rasmi wawe na uwezo wa kuoa au kuolewa(Capacity to marry), kwa maana ya umri na akili timamu.
Dhana ya ndoa ya udhani katika Sheria ya Ndoa ya 1971.
Sheria ya ndoa ya Tanzania inawachukulia watu ambao hawajaoana kihalali, kama watu wawili tofauti kabisa. Na sheria hii haijishughulishi kabisa watu wa aina hivi, isipokuwa tu katika mazingira fulani ambapo watu ambao hawajaoana kihalali wanaweza kuchukuliwa kuwa na ndoa au kudhaniwa kuwa na ndoa kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 160 na 160(1) cha Sheria hili. Ambavyo vimeeleza vigezo vya kufuata ili kuwe na dhanio la ndoa pasipo ndoa halali, kama ifuatavyo.
- Mwanaume na mwanamke lazima wawe wameishi pamoja chini ya Paa moja kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi.
- Wawili hao lazima wawe wanachukuliwa kama mke na mume katika jamii inayowazunguka, yaani wawe na utambulisho kama mke na mume katika jamii.
- Kuwe hakuna ndoa halali inayoendelea baina yao, au katika mmoja wao.
- Wawe na uwezo wa kuoa kwa mwanaume na kuolewa kwa mwanamke. Yaani mtu anayeishi na binti wa miaka 13 kwa mfano hakuwezi kuwa dhana ya ndoa hapo kwa binti hana uwezo wa kuolewa kutokana umri wake.
MUHIMU: Watu wengi hudhani kwamba dhana hii ya ndoa ya udhani, ni njia mojawapo ya ndoa ama kufikiri kuwa ni mbadala wa ndoa. La ha Sha si kweli kabisa, dhana hii si njia ya ndoa au si mbadala wa ndoa na hutumika tu pale ambapo kuna mgogoro na mmoja anakataa kuwa hapakuwa na ndoa au pale ambapo mmoja anafariki. Katika kulinda haki zao na watoto hapo ndio mahakama kwa kutumia vigezo tajwa hapo juu, hulazimika kutumia dhana hiyo ili kubatilisha uhusiano huo na kuweza kufanya mgawanyo wa mali na kuamua matunzo ya watoto.
Dhana hii pia inatambulika katika sheria za kimila Tanzania.
Namna ya kubatilishwa dhana ya Ndoa ya dhanio (presumption of marriage). Ndoa ya dhanio inaweza kubatilishwa pale ambapo kuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa, mwanaume na mwanamke wanaoishi pamoja hawakuwahi kufunga ndoa inayotambulika kisheria, na wala hawana cheti chochote cha ndoa. Katika muktadha huo jukumu la kuthibitisha (burden of proof) litakuwa kwa yule anayekataa kwamba kuna ndoa.
Katika kesi ya Raphael Libogo v. Wambura [1975]TLR No. 42
- Mwanamke na mwanaume waliishi pamoja kama mume na mke, na jamii ikawachukulia kama mke na mume, wakati fulani mmoja kati yao alikataa kuwepo kwa mahusiano hayo. Mahakama iliamua kwamba jukumu la kutoa ushahidi ni la yule anayekataa kuwepo kwa mahusiano.
MATOKEO YA KISHERIA YA KUBATILISHA DHANA YA NDOA YA DHANIO.
Kabla ya kuendelea mbele zaidi ni muhimu kutambua kubwa moja ya utofauti mkubwa uliopo kati ya Ndoa halali kisheria na Dhana ya Ndoa ya dhanio ni katika namna ya kuzivunja, katika ndoa halali, ndoa huvunjwa kwa TALAKA(DIVORCE), lakini katika dhana ya Ndoa ya dhanio, kwanza inatumika tu pakiwa na mgogoro lakini kuvunjwa kwake ni kwa KUBATILISHWA(REBUTTAL).
Kwa hiyo matokeo ya kubatilisha dhana ya Ndoa ya dhanio, yanafanana kabisa na matokeo ya kuvunja ndoa halali kisheria, nafuu zinazopatikana baada ya kubatilisha zinafanana na zile za talaka, na hii ndio lilikuwa lengo kuu, kulinda haki za watu wanaodhani wapo kwenye ndoa kumbe hawapo.
Kifungu cha 160(2) cha sheria ya Ndoa kisisitiza kwamba pale ambapo ndoa ya dhanio inabatilishwa na mahakama yenye mamlaka kufanya hivyo, mwanamke anahaki ya kuomba matunzo na matumizi kwa ajili yake na watoto wao.
Haki anazokiwanazo katika mambo kama matunzo, watoto wataishi na nani na mgawanyo wa mali zinafanana na zile za talaka katika ndoa halali. Katika kesi ya Andrew Martin v. Grace Christopher [2003], yafuatayo yalielezwa:-
- “Katika kesi hii mahakama ilisema kwamba, kwa kuwa Mkata rufaa na mjibu rufaa wameishi pamoja bila ndoa rasmi kwa takriban miaka 10, dhana ya Ndoa ya dhanio inaweza kubatilishwa, lakini mjibu rufaa anastahili haki zote na nafuu zote kama ambavyo zingepatikana kwa mwanamke mwingine ambaye ndoa yake halali kisheria ingevunjwa kwa talaka.”
Katika kuhitimisha makala hii ni muhimu kufahamu kuwa uhusiano wa kihawala au ndoa za Mitala yaani Concubinage association, hautambuliki na wala hauwezi kuingia katika dhana hii ya ndoa ya dhanio, hivyo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima ni muhimu kwa mwanaume na mwanamke wanaotaka kuishi pamoja kama mume na mke, kuhakikisha wanafunga ndoa kihalali inayotambulika kisheria, ili kulinda haki zao na watoto katika kipindi chote cha maisha yao na hata itakapotokea mivutano yoyote.

Discover more from ππππππππππβοΈ
Subscribe to get the latest posts sent to your email.

