SHERIA YA NDOA TANZANIA- SEHEMU YA 2.

MASHTAKA YA KINDOA(MATRIMONIAL LITIGATION).

Hizi ni taratibu ambapo upande mmoja wa ndoa awe mume ama mke, anakuwa na kesi dhidi ya upande mwingine kuhusu suala la kindoa. Taasisi kubwa mbili zenye mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya kindoa katika hatua tofauti ni:-

  • Mabaraza ya usuluhishi wa ndoa. (Marriage conciliatory boards) na,
  • Mahakama.

Mamlaka ya Mahakama(Jurisdiction of Courts).

Katika nchi yetu masuala ya kindoa na kifamilia husikilizwa katika mahakama za kawaida, tofauti na maeneo mengine ambapo huwa kuna mahakama maalumu za maswala ya kifamilia na kindoa, mahakama hizi huwa hazisikilizi kesi nyingine zozote, isipokuwa hizo tu. Hata hivyo mnamo mwaka 2021 mahakama ya Tanzania ilianzisha kituo jumuishi cha Temeke, katika mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza masuala ya familia, ndoa na mirathi.

Kituo jumuishi cha Temeke, kiliundwa kwa sababu zifuatazo:-

1. Kuharakisha Usikilizwaji wa Kesi za Familia na Mirathi โ€“ Kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, hasa zinazohusu ndoa, talaka, matunzo ya watoto, na mirathi.

2. Kutoa Huduma Jumuishi โ€“ Kituo kinajumuisha wadau mbalimbali kama Mahakama, Polisi, Ustawi wa Jamii, Dawati la Jinsia, na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kusaidia kesi za unyanyasaji wa kijinsia, haki za watoto, na masuala ya familia kwa ujumla.

3. Kuboresha Upatikanaji wa Haki kwa Wananchi โ€“ Kuleta huduma za kisheria karibu na wananchi, hasa wanawake na watoto ambao mara nyingi hukosa msaada wa kisheria katika migogoro ya kifamilia.

4. Kupunguza Ukali wa Kesi za Familia โ€“ Kusaidia kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya usuluhishi na si lazima kila kesi ipelekwe mahakamani.

5. Kutoa Msaada wa Kisaikolojia na Kisheria โ€“ Waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia na watoto wanaopitia migogoro ya familia wanapata msaada wa kisaikolojia, ushauri wa kisheria, na ulinzi unaohitajika.

Kwa ujumla, kituo hiki ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, hasa kwa makundi yaliyo hatarini kama wanawake na watoto. Hata hivyo kupitia makala hii LegalJamii inatoa wito kuongezwa kwa vituo hivi katika mikoa mingine, ili kurahisisha zaidi utoaji haki kama ilivyo kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Kifungu cha 76 cha sheria ya ndoa kinatoa mamlaka ya kwanza kusikiliza kesi(original jurisdiction) kwa mahakama ya mwanzo, Mahakama ya Wilaya, na  Mahakama ya Hakimu mkazi, Mahakama kuu, na Mahakama ya Rufani kama ifuatavyo;-

Katika nchi yetu ya  Tanzania, mamlaka ya mahakama katika kesi za ndoa inategemea aina ya ndoa na suala linalohusika. Sheria inayosimamia ndoa ni Sheria ya Ndoa ya 1971 (The Law of Marriage Act, 1971, Cap. 29). Mahakama zenye mamlaka ya kusikiliza kesi za ndoa ni:

(A). Mahakama ya Mwanzo

Inasikiliza migogoro ya ndoa na talaka ikiwa ndoa ni ya kimila au ya Kiislamu.(Customary or Islamic marriage)

Inaweza kutoa uamuzi juu ya matunzo ya watoto, mgawanyo wa mali, na talaka. Ikiwa mume na mke wameoana kwa ndoa ya Kikristo au ndoa ya kiserikali, Mahakama ya Mwanzo haina mamlaka ya kutoa talaka.


(B). Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya

Zina mamlaka ya kusikiliza migogoro yote ya ndoa, ikiwa ni pamoja na ndoa za kiserikali na Kikristo. Zinao uwezo wa kutoa talaka na kushughulikia mambo ya matunzo ya watoto na mgawanyo wa mali.


(C). Mahakama Kuu ya Tanzania.

Inasikiliza rufaa na kesi kubwa zaidi za ndoa, ikiwa ni pamoja na ndoa zilizofungwa kwa mujibu wa sheria rasmi. Inayo mamlaka ya kutoa talaka, kugawa mali, na kuamua matunzo ya watoto katika ndoa zote zilizosajiliwa.

(D). Mahakama ya Rufaa ya Tanzania

Inasikiliza rufaa kutoka Mahakama Kuu kuhusiana na kesi za ndoa.


Kwa hivyo kwa ujumla masuala Yanayoshughulikiwa na Mahakama katika Kesi za Ndoa ni:-

1. Talaka na Ubatilishaji wa Ndoa

2. Mgawanyo wa Mali Baada ya Talaka

3. Matunzo ya Watoto

4. Haki za Mke na Mume

MABARAZA YA USULUHISHI WA NDOA. (MARRIAGE CONCILIATORY BOARDS)

Haya ni mabaraza yaliyoanzishwa chini ya sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 chini ya kifungu cha 102, ambapo mabaraza haya yanajumuisha mabaraza ya kidini, mabaraza ya kimila na mabaraza ya serikali za mtaa, lengo la kuundwa kwa mabaraza haya ni kusaidia wanandoa kuelewana, kusuluhishana na kupatana bila ya kufikisha kesi mahakamani. Vilevile yalilenga kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani mahakamani, kwani kama wanandoa wakipatana hawatakuwa na haja ya kwenda mahakamani.

Ni takwa la lazima kwa kila shauri la ndoa kupitia kwanza kwenye baraza la usuluhishi wa Ndoa kabla ya kupelekwa mahakamani, chini ya kifungu cha 101 cha Sheria ya Ndoa ya 1971. Hata hivyo ni muhimu kutambua kuwa mabaraza haya hayana mamlaka ya kutenganisha wanandoa au kutoa talaka, kazi yao ni usuluhishi tu.

  • Iwapo baraza la usuluhishi litashindwa kusuluhisha, linapaswa kutoa Cheti cha kuonyesha kushindwa kwake kutatua shauri hilo. Kifungu cha 101(2) cha sheria ya ndoa kinasema Maombi ya talaka lazima yaambatanishwe na Cheti cha baraza la usuluhishi na yawasilishwe katika kipindi kisichopungua miezi sita.
  • Maombi ya talaka yakipelekwa mahakamani bila kupitia kwenye baraza la usuluhishi wa ndoa, yatakuwa batili, kama ilivyoelezwa katika kesi ya SHILO MZEE v. FATUMA AHMED[1984] TLR 112.
  • Hata hivyo yako mazingira ambayo cheti kinaweza kisitumike katika baadhi ya kesi. Ambapo mazingira ya kufanya usuluhi huwa yanakuwa magumu. Mfano, kama ndoa imesajiliwa nje ya Tanzania, ikiwa mmoja wa wanandoa amepotea kwa muda mrefu, au amefungwa gerezani kwa muda mrefu, au iwapo kuna unyanyasaji mkubwa wa wazi dhidi ya mwanandoa mmoja, ama kama mmoja ameugua ugonjwa wa akili (mental illness).

MUUNDO NA MAMLAKA YA MABARAZA YA USULUHISHI.

Kwa mujibu wa kifungu cha 103 cha sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza kuwa baraza litaundwa na Mwenyekiti na watu wasiopungua watano. Hakuna mwakilishi wa kisheria atakayeruhusiwa, isipokuwa mwanandoa anaweza kusindikizwa na rafiki au mwanafamilia.

Baraza litasuluhisha tu mashauri ya wanandoa wanaoishi katika maeneo yake husika, katika kata husika. Na mabaraza ya kidini yanamamlaka ya kusuluhisha wanandoa ambao ni wa dini moja.

IKUMBUKWE: Mabaraza haya yanapaswa kusajiliwa na kutambuliwa rasmi kama yenye uwezo wa kusuluhisha na Ofisi ya mkuu wa wilaya. Si kila baraza linauwezo wa kusuluhisha.

Iwapo baraza litafanikiwa kusuluhisha, mgogoro utaishia pale, lakini likishindwa mgogoro huo utapelekwa mahakamani.

NAFUU KATIKA MASHAURI YA KINDOA.

  1. Amri ya Tamko- hii ni amri inayoombwa na kutoelewa na mahakama ili kutangaza au kuelezea jambo fulani ambalo lilikuwa na utata, ili kuondoa utata. mfano mahakama inaweza kutamka kwamba mali fulani ni mali ya Wanandoa wote na si mwanandoa mmoja pekee.
  2. Amri ya kubatilisha- hii ni amri itolewayo na mahakama, ikiwa itaombwa na upande mmoja wa ndoa wa kubatilisha ndoa ambayo haikuwa halali kisheria. Ikiwa mahakama itajiridhisha itatoa amri hiyo.
  3. Amri ya kutengana kimahakama – kifungu cha 110 cha Sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza kuwa mahakama inaweza kutoa amri ya kutengana kwa wanandoa kuishi tofauti, kwa kuondoa jukumu la kuishi katika nyumba moja na chini ya paa moja, lakini inaweza kubakiza haki nyingine za kindoa yaani Consortium rights.

Mambo ya kuzingatia katika Kutoa amri ya kutengana.

(A). Ndoa lazima iwe katika mgawanyiko (broken down)- kifungu cha 99 na 110(1) cha sheria ya Ndoa kinaeleza kuwa ili amri ya kutenganisha wanandoa iweze kutolewa ni lazima kuzingatia kuwa wanandoa hao wapo kwenye mgawanyiko, na kwamba endapo wataendelea kukaa chini ya paa moja haki za mmoja wao zinaweza kuvunjwa. Ni muhimu kuzingatia kuwa KUTENGANA SI KUACHANA. Lakini ili kujua kuwa ndoa ipo kwenye mgawanyiko mambo yafuatayo yanapaswa kutazamwa kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 107(2) cha Sheria ya Ndoa.

(I). Uzinzi/fumanizi kwa mwanandoa

(II). Unyanyasaji wa kingono mfano mwanandoa mmoja kutaka kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

(III). Ukatili ama wa kimwili au wa kiakili kwa mwanandoa mwenzake au watoto.

(IV). Kutelekeza familia bila huduma zozote za kiafya au kijamii kwa kipindi kisichopungua miaka 3

(V). Kumtenga kwa makusudi mwanandoa na kushindwa kumhudumia.

(VI). Iwapo kutengana huko kwa wanandoa ni kwa hiari ama kwa amri ya mahakama.

MUHIMU: Mambo haya tajwa hapo juu yanayotumika kubaini iwapo ndoa ipo kwenye mgawanyiko, yanafanana na yale yanayotumika katika Talaka.

(B). Kifungo cha mwanandoa mmoja ama cha maisha au cha miaka isiyopungua mitano.

(C). Ugonjwa wa akili kwa mwanandoa mmoja, ambao umethibitishwa angalau na madaktari wawili.

(D). Kubadili dini kwa mwanandoa.

Mambo hayo yote yanapaswa kubainishwa na mahakama kabla ya kutoa amri ya kutenganisha wanandoa, mwanandoa anayeoomba amri ya kutengana anapaswa kuthibitisha kuwa anatendewa mambo hayo na mwanandoa mwenzake.

MATOKEO YA KISHERIA YA KUTENGANA.

Kisheria amri ya kutengana haiuwi au kumaliza ndoa, isipokuwa inaondoa jukumu la kuishi pamoja chini ya paa moja (duty to cohabit),Consortium pamoja na ridhaa ya kushiriki tendo la ndoa ya moja kwa moja. Katika kutengana wanandoa wanaweza kuwa na makubaliano fulani ambayo baadae hupitishwa na mahakama na kuwa amri. Iwapo wanandoa watashindwa kufikia makubaliano mahakama itatoa amri katika mambo ya msingi yafuatayo:-

  • Matunzo
  • Watoto wataishi na nani, kifungu cha 110(3) cha sheria ya Ndoa.
  • Haki ya kuwaona watoto/ kuwatembelea watoto.
  • Kukomesha unyanyasaji

Kutengana kwa wanandoa kisheria, si jambo la kudumu linapaswa kuwa jambo la muda mfupi tu, ambalo litamalizwa kwa ama Talaka au kuungana tena kwa wanandoa kwa kumaliza tofauti zao ili waishi kwa furaha. Kifungu cha 113(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971.

KUVUNJIKA KWA NDOA.

Dissolution of marriage.

Kama tulivyoeleza katika sehemu ya kwanza ya makala hii, ndoa ni muunganiko wa hiari wa mwanaume na mwanamke kuisha pamoja kama mume na mke, muungano huu umekusudiwa kuwa wa milele. Lakini kama binadamu tunakumbana na vikwazo na changamoto mbalimbali ambazo mwanandoa mmoja anaweza kushindwa kuhimili, na kutaka kuvunja ndoa. Yafuatayo ni mazingira ambayo hakutakuwa na namna nyingine isipokuwa kuvunja ndoa:-

  1. Kifo cha mmoja wa wanandoa, hii hufanya ndoa kufika mwisho na kumwacha mwanandoa aliyesalia kuwa huru, na kuweza kuoa tena.
  2. Amri ya kuwepo kwa dhana ya  kifo kwa mwanandoa mmoja, ambayo sheria inaruhusu kuomba amri hii, iwapo mwanandoa mmoja hajaonekana kwa kipindi cha miaka 5 au zaidi, pamoja na jitihada zote za kumtafuta.hii pia huweza kuvunja ndoa kifungu cha 161, 94(2)e na 95 cha Sheria ya Ndoa ya 1971.
  3. Amri ya Talaka inayotolewa na mahakama baada ya kuombwa na mwanandoa mmoja, kama mahakama itajiridhisha kuwa ndoa hiyo imegawanyika na haiwezi kurekebishika tena. (The marriage is broken down, irreparably, beyond repair)

Ni muhimu kukumbuka kuwa SEPARATION haivunji Ndoa, lakini DIVORCE inavunja ndoa.

Utajuaje ikiwa ndoa hii, imegawanyika na haiwezi kurekebishika?

Vigezo ni vilevile kama ambavyo vimetajwa kwenye kutenganisha isipokuwa tofauti ni kiwango, huku kwenye Talaka vitendo hivyo vinakuwa vimezidi na visivyohimilika.

Uzinzi/fumanizi.(Adultery)

Hii ni hali ya kufanya mapenzi kati ya mwanamume na mwanamke ambao si wanandoa, wakati kukiwa na ndoa inayoendelea miongoni mwa mmoja wa wanandoa hao, au wote wakiwa na ndoa zao tofauti.

Namna ya kuthibitisha uzinzi.

Mara nyingi huwezi kuthibitisha uzinzi kama hakuna penetration yaani kitendo cha uume kuingia kwenye uke), na si lazima kitendo chote kufanyika penetration tu inatosha kuwa uzinzi, ni Ngumu kukana kuwepo kwa uzinzi isipokuwa tu kama mwanaume ana uonji (impotence) hapo hakutakuwa na fumanizi. Hata hivyo kutokana na kuwa ngumu sana kupatikana kwa ushahidi wa moja kwa moja katika uzinzi, unashahidi wa kimazingira unaweza kukubalika kulingana na kesi itakavyokuwa.

Mambo mengine yanaweza kuwa ukatili, Kutekeleza mwenza ukiwa na nia ya kusalia mwenyewe daima na bila sababu za kueleweka, na unyanyasaji.

Amri ya Talaka inaweza isitolewe na mahakama iwapo mambo yafuatayo hayatafuatwa:-

  • Kama hakutakuwa na cheti kutoka baraza la usuluhishi wa ndoa kuonyesha kuwa wameshindwa kusuluhisha, cheti ambacho kinapaswa kuambatanishwa kwenye Maombi ya talaka, hii pia ilielezwa katika kesi ya ATANASI MAKUNGWA v. DOREEN.
  • Iwapo ndoa itakuwa haijadumu kwa kipindi cha miaka 2, kifungu cha 100 cha sheria ya ndoa kinaeleza kuwa ili mwanandoa aweze kuomba talaka ni lazima ndoa hiyo iwe imedumu angalau kwa miaka 2, chini ya miaka 2 mwanandoa atakuwa hajakidhi kuomba talaka. Hata hivyo kifungu cha 100(2) kinaeleza mazingira ambayo wanandoa wanaweza kuomba talaka hata chini ya miaka 2 mathalani mateso yaliyopitiliza.
  • Iwapo ndoa itakuwa haijagawanyika katika kiwango cha kushindwa kurekebishika.
  • Ikiwa maombi ya talaka, yatatokana na makosa ya mleta maombi mwenyewe.

Mambo (3)matatu ambayo yakifanywa na mwanandoa yatamzuia na kumnyima haki ya kuomba talaka.

  1. Makubaliano ya kudanganya au kuficha taarifa muhimu, iwapo mwanandoa anayetarajia kuomba talaka atakubaliana na mwenzake kuficha taarifa au kudanganya, atakuwa amejiondolea haki ya kuomba talaka.
  2. Iwapo mwanandoa atasamehe kosa kubwa la kindoa(condonation) ambapo ni lazima awe ana fahamu kuhusu kosa hilo na nia ya kusamehe ifahamike kwa wanandoa wote. Kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 86 cha sheria ya Ndoa 1971.
  3. Iwapo mwanandoa mmoja ataonyesha tabia ya kumshawishi, ama kumpelekea mwenzake kufanya kosa la kindoa.(Connivance). Mfano  iwapo mwanandoa mmoja atamnyima mwenzake unyumba, kwa makusudi na kumfanya mwenzake kufanya uzinzi. Kifungu cha 85 cha sheria ya Ndoa ya 1971

Extra judicial divorces.

Hii ni talaka isiyotolewa na mahakama, yaani hutolewa kwa utaratibu wa nje ya mahakama ama wa kidini au kitamaduni. Talaka hizi pia hutambuliwa na mahakama na zina utaratibu wake ambao husaidia mahakama kufikia katika maamuzi sahihi ya kuvunja ndoa za aina hii.

MGAWANYO WA MALI.

Baada ya amri ya talaka kutolewa hatua inayofuata huwa ni mgawanyo wa mali za wanandoa(Matrimonial properties), kwa Tanzania mahakama haiwezi kugawanya mali wakati ndoa bado inaendelea, ni lazima talaka itolewe kwanza. Kifungu cha 114 na 106(a) cha sheria ya Ndoa 1971 kinaeleza kuwa ni jukumu la kugawanya mali kisheria ni la Mahakama. Mgawanyo wa mali lazima uombwe na mwanandoa katika maombi ya talaka.

Mahakama lazima izingatie yafuatayo:-

(A). Mgawanyo lazima uwe baada ya kutolewa kwa talaka.

(B). Lazima kuwe na maombi ya mgawanyo wa mali, kutoka kwa mwanandoa anayeomba talaka.

(C). Mgawanyo lazima uwe kwenye mali zile zilizochumwa na kutafutwa na wanandoa wote kwa pamoja, wakati wa ndoa. Kwa jitihada za mume na mke.

Katika kesi ya BI. HAWA MOHAMED V. ALLY SEIF[1983] TLR ukurasa wa 2 imeeleza yafuatayo;-

  • Nini maana ya jitihada za pamoja, jitihada za pamoja ni shughuli zozote zinazochangia katika ustawi wa familia.
  • Kwamba ni muhimu kuzingatia kiwango cha mchango au jitihada katika kupata mali, ni kwa kiasi gani wanandoa wamechangia kila mmoja katika kupata mali. Kwa hiyo hapa si tu suala la nusu kwa nusu kama ambavyo wengi hudhani, kiwango cha uchangiaji ni lazima kitazingatiwa.
  • Katika kugawanya mali ni muhimu pia kuzingatia mila na desturi za jamii wanazotoka wanandoa hao.
  • Katika mgawanyo wa mali pia ni muhimu kuzingatia madeni waliyokuwa nayo wanandoa, madeni au mikopo ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya familia.
  • Ni muhimu pia kuzingatia mahitaji ya watoto wa wanandoa, kwa ajili ya ustawi wao hususani wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
  • Matunzo ya watoto na mahali watakapo kaa,yaani custody of the Children. Kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 04(2) cha sheria ya Mtoto ya 2009 na kifungu cha 135 cha sheria ya Ndoa ya 1971. Ambapo katika suala la watoto watakaa na nani ni muhimu kuzingatia Maoni ya watoto, wazazi, uwezo wao kiuchumi, umri wa watoto.

Katika kuhitimisha makala hii, ni vizuri ikafahamika kwamba kwa ujumla kuvunja ndoa ni jambo baya, na ni jambo ambalo kila wanandoa wanapaswa kujitahidi kuliepuka kwa sababu madhara yake ni makubwa sana hasa kwa watoto. Hata hivyo kidini pia talaka ni jambo ambalo halimpendezi Mwenyezi Mungu, kwa sababu ni utengano. Lakini kama tulivyoangazia hapo awali yako mambo yanayoweza kutokea na kusababisha wanandoa kushindwa kabisa kuvumiliana na kuhimili, na katika hali hiyo endapo usuluhishi utashindikana ili kurekebisha ndoa hiyo basi hakutakuwa na budi kutoa talaka.


Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Published by LEGALJAMIIโš–๏ธ

Richard Kalokola is a Tanzanian legal professional with a Bachelor of Laws (LL.B) from St. Augustine University of Tanzania and professional training from the Law School of Tanzania. He has a strong passion for legal education, research, and public legal awareness. As the founder of LegalJamii, Richard is dedicated to bridging the gap between complex legal principles and everyday understanding by delivering accurate, practical, and accessible legal information. His vision is to promote a legally informed society where individuals, businesses, and communities can confidently understand their rights, responsibilities, and available legal solutions. Through LegalJamii, he continues to advance legal literacy by transforming legal concepts into clear and simplified language for the benefit of the wider public.

One thought on “SHERIA YA NDOA TANZANIA- SEHEMU YA 2.

Leave a Reply

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading