SHERIA YA NDOA TANZANIA- SEHEMU YA 1.

MAANA YA FAMILIA.

Familia ni dhana pana sana yenye tafsiri tofauti tofauti kulingana na mazingira, lakini katika tafsiri ya msingi familia ni muunganiko wa watu, ambao wanahusiana kwa damu, ndoa au kuasiliwa.

Familia ni kundi la watu wanaohusiana kwa damu, ndoa, au uhusiano wa kulea, wanaoishi pamoja au kushirikiana kwa namna fulani katika maisha yao. Kwa kawaida, familia hujumuisha wazazi na watoto wao, lakini inaweza pia kuwa pana zaidi na kujumuisha ndugu, babu, bibi, wajomba, shangazi, binamu, na hata marafiki wa karibu wanaochukuliwa kama sehemu ya familia. Kwa namna iliyozoeleka familia ni Baba, Mama na Watoto.

SHERIA YA FAMILIA.

Hili ni tawi la sheria ambalo linashughulika na mambo yanayohusu mahusiano ya kifamilia kama vile Ndoa, talaka, haki za wanandoa, matunzo ya watoto na watoto wataishi na nani? Katika Nchi yetu sheria kuu inayoongoza masuala ya ndoa na familia ni SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971. (The Marriage Act of 1971). Hata hivyo zipo sheria nyingine ambazo pia hutumika kwa Pamoja kama vile, SHERIA YA MTOTO YA MWAKA 2009, SHERIA YA ARDHI YA MWAKA 1999, KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977 na marekebisho yake mbalimbali, Pamoja na Sheria za kimila. Sheria ya mtoto ya Mwaka 2009 katika kifungu cha 3 imetoa maana ya kisheria ya Familia kwa maana ifuatayo:-

  • “Mzazi mama au Baba na watoto wanaolelewa au wenye uhusiano wa damu na ndugu wengine wa karibu wanaojumuisha babu, bibi, wajomba, mashangazi, binamu na wapwa wanaoishi kwenye nyumba.”

Historia ya Sheria ya Ndoa Tanzania inaweza kuangaziwa kabla ya mwaka 1971 ambapo, hapakuwa na sheria moja jumuishi inayoongoza masuala ya ndoa, lakini baada ya kutungwa kwa sheria ya ndoa mwaka 1971 kulijitokeza uhitaji wa kuunganisha sheria zote za ndoa za Afrika Mashariki, ambayo ilichochewa na mgongano na ugumu kati ya sheria za Nchi na zile za kidini, kuhusu namna gani ndoa inapaswa kuwa.

NDOA NA UUNDWAJI WAKE.

Ndoa ni nini?

  • Ndoa ni muungano wa hiari na wa kisheria wa watu wawili, mwanaume na mwanamke wanaokubaliana kuishi kama mume na mke. Kwa upande mwingine ndoa inachukuliwa kubwa muungano tukufu. Vilevile ndoa inachukuliwa kubwa ndio kiini cha familia.
  • Ndoa pia inabeba dhima na maana tofauti kulingana na jamii, watu, dini na tamaduni ambazo huwa na mitazamo tofauti. Mfano:- WAHINDU wanachukulia ndoa kama Muungano wa milele hata baada ya kifo, WAKRISTO wanachukulia ndoa kama muungano wa kisakramenti na hivyo mtakatifu, wa kudumu na usioweza kuvunjika. WAISLAMU huchukulia ndoa kama Muungano wa kiraia na unaweza kuvunjwa kukitokea kutokuelewana kusiko rekebishika kwa wanandoa. Kwa mujibu wa Dini ya kiislamu ndoa ni tendo la kimungu (ibadat) na la kibinadamu (muamalat).
  • Kisheria ni ngumu kuwa na tafsiri ya moja kwa moja ya ndoa lakini angalau ipo msamiati ya msingi ambayo inategemewa kukutwa kwenye kila tafsiri ya ndoa kisheria ambayo ni “Muungano wa hiari baina ya mwanamume na mwanamke, kuishi kama mume na mke”

NAMNA YA KUANZISHA UHUSIANO WA KINDOA.

Hakuna namna ya kisheria ya moja kwa moja ya namna ya kuanzisha mahusiano ya kindoa, lakini sheria ya Ndoa ya 1971 kifungu cha 18(1) kinawataka watu wanaokusudia kuoana kutoa Notisi ya nia yao kwa msajili, notisi hiyo inapaswa kusajiliwa siku 21 kabla ya siku ya ndoa na msajili ataichapisha kwa umma. Ili notisi hiyo ikubaliwe yako mambo kadhaa ya kuzingatiwa ikiwemo umri, ridhaa ya wazazi au walezi na mahusiano hayo yasiwe yamekatazwa kisheria.(Prohibited relationship)

Kwa Kutoa mahali. Mara nyingi kwa sheria za kimila, mahusiano ya kindoa kuanzishwa kwa upande wa mwanaume kutoa mahali kwa upande wa mwanamke, ambayo utaratibu wake hutofautiana kulingana na tamaduni za jamii husika.

Kwa kuvishana Pete. Kwa sheria ya kiingereza watu wawili yaani mwanaume na mwanamke wanaweza kuanzisha uhusiano wa kindoa kwa kuvalishana pete (engagement ring) katika ahadi ya kumuoa mtu.

Sheria za Tanzania hazijazungumzia kuhusu mkataba wa kuoa, bali zimezungumza zaidi kuhusu Ahadi ya kuoa(promise to Marry) na inajumuisha wajibu ambao unapaswa kutekelezwa na kama ilipotekelezwa unaweza kuleta madhara kisheria, kifungu cha 69 cha sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza kwa kina.

Ahadi ya ndoa inaweza kuwa ya moja kwa moja kwa maana ya mwanamume kumueleza mwanamke atamuoa kwa mdomo, au Ahadi inaweza kuwa si ya moja kwa moja bali kwa kuzingatia matendo ya wachumba. Mfano matendo kama kununua fanicha, jiko na vitu kama mapazia na kushauriana pamoja namna ya kupanga vitu hivyo katika nyumba, kupeana zawadi zinazoashiria kuwa wachumba watakuwa mke na mume.

Ahadi hii ya kuoa lazima iwe katika ya wachumba ambao wamekubaliana kwa masharti yanayofanana na yanayopaswa kueleweka baina yao katika namna yoyote iliyotumika. Aidha inapaswa kuwa huru bila kushurutishwa au kulazimishwa na kuwa halali.

KUVUNJA AHADI YA KUOA.

Iwapo ahadi ya kuoa (promise to Marry) itavunjwa na upande wowote inaweza kuleta madhara kisheria na kupelekea malipo ya fidia. Na inatokea pale ambapo mmoja kati ya wachumba anashinda kutimiza ahadi yake.

Upande ulioumizwa na kutotimizwa kwa ahadi ya kuoa unaweza kushtaki kwa ajili ya kupata fidia, hata hivyo upande huu hauwezi kudai specific performance ya ahadi ya kuoa kwa sababu ndoa ni muungano wa hiari kwa hivyo hauwezi kulazimishwa.kifungu cha 70 cha sheria ya Ndoa ya 1971 kinatoa ukomo wa muda wa mtu kupeleka malalamiko ya kuvunjwa kwa ahadi ya kuoa kuwa Mwaka mmoja toka siku ahadi hiyo ilipovunjwa.

  • Katika kesi ya Mohamed Simonio v. Sophia Msingi[1975] HCD, Sophia alimshtaki Mohamed akidai fidia ya TZS 25,000/= kwa kuvunja ahadi ya kumuoa, na kusababisha yeye kupoteza kazi kwa kupata ujauzito na kwamba hisia zake ziliumizwa. Mahakama ya wilaya iliamua kuwa Sophia alipwe TZS 25,000/= kwani kweli kulikuwa na uvunjifu wa ahadi ya kumuoa, lakini katika Rufaa Mahakama kuu ilipunguza fidia hiyo hadi TZS 20,000/= kwa sababu kupata ujauzito si miongoni mwao sababu za kisheria za kumuachisha kazi mtu.

NI VIPI VIGEZO VYA NDOA HALALI KISHERIA.

Kimsingi vipo vigezo takribani vitano vya ndoa halali mbele ya macho ya sheria. Lakini ni muhimu kutambua kuwa ndoa halali lazima iwe ya HIARI, lazima iwe katika MWANAUME NA MWANAMKE, na ikusudiwe kuwa ya MILELE. Vigezo vingine ni kama ifuatavyo:-

  1. Uwezo wa Kuoa/kuolewa.(Capacity to Marry). – Hapa tunazungumzia mambo muhimu UMRI wa kuoa kwa mwanaume ambao ni miaka 18 na mwanamke miaka 15, hata hivyo mtu ambaye yupo chini ya umri huo anaweza kuoa/kuolewa lakini lazima kuwe na ridhaa(consent) ya wazazi/walezi au Mahakama, kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Ndoa ya 1971.
  • Umri wa kuoa au kuolewa hutofautiana pia kutokana na Dini mathalani dini ya Kiislam wao wanaamini kwa mwanaume akifikisha baleghe anakuwa tayari kuoa, wakati msichana wa miaka 14 anaweza pia kuolewa kwa ridhaa ya wazazi/walezi, hapa ndipo huwa mjadala mkubwa unaibuka hususani kwa wanaharakati wa haki za watoto, kwa sababu kwa mujibu wa sheria ya mtoto 2009, mtoto ni mtu mwenye umri chini ya Miaka 18 kwa hiyo kwa sheria hii ya Ndoa, huchukuliwa kama inaunga mkono ndoa za utotoni.
  • Yasiwe mahusiano yaliyozuiwa kisheria(Prohibited relationship), ili ndoa iweze kuwa halali kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha sheria ya Ndoa ya 1971, yanapaswa kubwa kuwa mahusiano ambayo hayajazuiwa kisheria mfano wa mahusiano yaliyozuiwa ni kama Mtoto na mzazi, Kaka na Dada, mtoto wa nje ya ndoa wa mmoja wa wanandoa na mtoto wa ndani ya ndoa au mtoto wa kuasiliwa/kulelewa.
  • Kusiwe na ndoa inayoendelea (subsisting Marriage), kifungu cha 15 cha sheria ya Ndoa ya 1971, kinakataza mtu yeyote kuingia kwenye ndoa mpya ikiwa bado ana ndoa nyingine inaendelea na haijavunjwa kisheria. Isipokuwa tu kwa wale wanaoruhusiwa kufunga ndoa zaidi ya mara moja(Polygamy) hususani waislamu.

2. Notisi ya siku 21.

  • Ndoa halali kisheria lazima izingatie kutoa notisi ya siku 21 kabla ya siku ya harusi kwa msajili, hata hivyo yapo mazingira ambayo utaratibu wa notisi ya siku 21 unaweza usifuatwe na halali ikafungwa katika mazingira hayo ni lazima msajili ajiridhishe kwamba wanandoa watarajiwa wanao uwezo wa kuoa/kuolewa kama ilivyoelezwa hapo. Haya yanapatikana katika kifungu cha 23 cha sheria ya Ndoa 1971.

3. Mashahidi wawili au Zaidi.

Ili ndoa iwe halali ni lazima ishuhudiwe na watu wawili au zaidi, mashahidi hao wanapaswa kuwa na umri wa miaka 18 au Zaidi, wenye akili timamu na wanaoelewa lugha inayotumika katika sherehe ya ndoa. Hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria ya Ndoa ya 1971.

4. Ndoa halali ni lazima ifungwe mbele ya umma, yaani mbele ya watu au inaweza kufungwa kwenye ofisi ya Msajili, kama ni ya kikristo ifungwe kanisani au mahali pengine kwa mujibu wa utaratibu wa RITA kama iliandikwa kwenye kifungu cha 28 na 30(1) cha Sheria ya Ndoa ya 1971.

5. Msingi mwingine wa ndoa halali hasa kwa ndoa za kikristo, ni lazima pande zote mbili kwa maana ya mwanadamu na mwanamke wawepo wenyewe siku ya kufunga ndoa na harusi, hairuhusiwi kuwakilishwa yaani bwana harusi au bibi harusi hawezi kuwakilishwa na mtu mwingine siku ya ndoa. Hiyo ni kulingana na kifungu cha 28(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971.

INGAWAJE

Katika sheria za Kiislamu, ndoa ni mkataba wa kihalali unaohitaji ridhaa ya wahusika wote wawiliโ€”bwana harusi na bibi harusi. Ndoa ya kiislamu pia hujulikana kama Nikah. Hata hivyo, sheria za Kiislamu zinaeleza kuwa ndoa inaweza kufungwa kwa kutumia mwakilishi (wakili) katika hali fulani.

Sheria za Kiislamu Kuhusu Uwakilishi Katika Ndoa

Kwa mujibu wa Fiqh ya Kiislamu, bibi harusi anaweza kuwakilishwa na wali (mlezi wake wa ndoa), kama vile baba, mjomba, au ndugu wa kiume wa karibu, ikiwa ni kwa ridhaa yake. Pia, bwana harusi anaweza kumteua mwakilishi (wakil) ili kumwakilisha katika kufunga ndoa ikiwa hana uwezo wa kuhudhuria kwa sababu halali.

Sheria za Tanzania Kuhusu Ndoa za Kiislamu

Katika sheria za Tanzania, ndoa za Kiislamu zinafuata misingi ya Shariah, lakini pia zinapaswa kuzingatia Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya 1971. Sheria hii haitaji moja kwa moja uwezekano wa uwakilishi katika ndoa, lakini inatambua ndoa za dini kama halali iwapo zimefungwa kwa mujibu wa imani hiyo.

Kwa hivyo, katika ndoa ya Kiislamu inayofungwa Tanzania:

Bibi harusi anaweza kuwakilishwa na wali wake, lakini anapaswa kutoa ridhaa yake wazi.

Bwana harusi anaweza kuwakilishwa na wakili wake, mradi tu ridhaa yake imethibitishwa.

Uwakilishi huu unapaswa kufanyika kwa mujibu wa taratibu za Kiislamu, kama vile kufanywa mbele ya mashahidi wawili wa Kiislamu na kadhi au sheikh anayefungisha ndoa.

AINA ZA NDOA.

Kuna Aina kuu mbili za Ndoa kama ilivyotajwa katika kifungu cha 10 cha sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

  1. Ndoa ya Mume mmoja na mke mmoja(Monogamous Marriage)
  2. Ndoa ya Mume mmoja na wake wengi (Polygamous Marriage)

AINA ZA KUSHEREHEKEA NDOA.

Kwa Mujibu wa kifungu cha 25(1) cha sheria ya ndoa ya 1971 sherehe za ndoa zinatambuliwa katika aina zifuatazo, sherehe za Ndoa ya Bomani/Ndoa ya kiserikali, Kikristo, kiislamu na kitamaduni

1. Ndoa ya kimila โ€“ Hii ni ndoa inayofungwa kwa kufuata mila na desturi za makabila mbalimbali nchini Tanzania. Inaweza kuhusisha mahari na taratibu nyingine za kimila, lakini lazima iheshimu sheria za ndoa za Tanzania.


2. Ndoa ya kiserikali (civil marriage) โ€“ Hii ni ndoa inayofungwa mbele ya msajili wa ndoa katika ofisi za serikali. Inahusu zaidi wale ambao hawataki ndoa ya kidini au kimila na inafuata taratibu rasmi za kisheria kama ilivyotajwa katika kifungu cha 29 cha sheria ya Ndoa ya 1971. Ndoa hii ni maarufu kwa jina la ndoa ya Bomani

3. Ndoa ya kidini โ€“ Hii ni ndoa inayofungwa kwa mujibu wa taratibu za dini na imani ya Dini hizo, kama vile Uislamu, Ukristo, au dini nyingine zinazotambulika. Lazima ifungwe na kiongozi wa dini anayesajili ndoa hizo. Na hapa ni muhimu kusisitiza kuwa mtu/mchungaji kwa wakristo anayefungisha ndoa hii anapaswa kuwa na leseni ya kufanya hivyo, kama inavyoelezwa katika kifungu cha 30(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971. Kwa Waislamu ndoa hufungishwa na kadhi, shekhe.

Vizuizi vya Ndoa(Marriage Restrictions).

Yapo mazingira fulani ambayo yakitokea ndoa halali haiwezi kufungwa, na ikitokea ndoa imefungwa pamoja na kuwepo kwa mazingira hayo basi haitahesabiwa kuwa ndoa Halali kisheria. Kwa hiyo mambo hayo kama tulivoyatazama huko awali ikiwemo kuwepo kwa ndoa halali inayoendelea, kuwa katika mahusiano batili, na kutokuwa na uwezo wa kuoa/kuolewa  ndiyo huunda vikwazo hivyo vya ndoa ndiyo maana kukawepo utaratibu wa notisi ya siku 21 ili yeyote mwenye pingamizi la haki aliwasilishe.

MATOKEO YA KISHERIA YA KUFUNGA NDOA.

Hapa tutaangazia nini kinatokea baada ya kufunga ndoa kisheria? Pale watu wanapooana kihalali kwa kufuata sheria, huwa wanatengeza haki na kupata wajibu kwao wenyewe na hata watu wengine katika jamii. Kwa hivyo matokeo ya kisheria ya kufunga ndoa kimsingi ni kuanza kwa haki na wajibu baina ya wanandoa na hata jamii kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 16(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971.

Haki na wajibu wa wanandoa.

  • Chini ya sheria ya kiingereza ya Common Law wakati wa nyuma jukumu la kwanza la wanandoa lilikuwa ni jukumu la kuishi pamoja chini ya paa moja(Cohabitation), jukumu lililoenda sambamba na haki ya wanandoa iitwayo Consortium, ambayo inajumuisha haki ya wanandoa kusaidiana, haki ya kupendana, haki ya unyumba, haki ya kutumia jina la mume, haki ya kuwa na makao ya familia (matrimonial home) na haki ya kutunziana siri za ndoa. Kwa wakati huo ilikuwa ni jukumu na mke kumfuata mume na kuishi naye katika nyumba yake, lakini kutokana na mabadiliko ya sheria hizo hizo Mke sasa hatazamwi tena kama upande dhaifu katika ndoa, bali mume na mke wana haki sawa na SASA MUME NA MKE NI WATU WAWILI TOFAUTI KISHERIA, kwa maana kila mmoja kuwa na uwezo wa kumiliki mali zake binafsi na kila mmoja kuweza kuweza kushtaki au kushtakiwa kwa jina lake.
  • Chini ya Sheria ya Ndoa ya 1971, hakuna kifungu maalum kinachoeleza wazi kuhusu jukumu la kuishi pamoja chini ya paa moja (Cohabitation), hata hivyo inaelezwa kuwa jukumu hilo limeelezwa katika namna isiyo ya moja kwa moja chini ya kifungu cha 111 na 67 ambayo inaeleza uwezekano wa wanandoa kuishi tofauti kwa makubaliano ya maandishi. Kifungu cha 140 kinazuia mahakama kulazimisha wanandoa kuishi pamoja chini ya paa moja, isipokuwa kama itagusa maslahi ya watoto. Jukumu la kuishi pamoja chini ya paa moja sio la lazima.

1.Wajibu wa matunzo.

Ni wajibu wa kisheria wa mume kumtunza mke au wake zake.huu ni wajibu wa kumpatia mke mahitaji ya msingi. Wajibu huu unaendana pia na uwezo wa kiuchumi wa Mume. Mke anaweza kuwa na wajibu huo iwapo tu anao uwezo wa kufanya hivyo, na kwamba Mume hana uwezo wa kutunza kutokana na ugonjwa. Kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 63 cha sheria ya Ndoa. Jukumu hili linaweza kuachwa ambapo wanandoa wanatengana kwa makubaliano au amri ya mahakama.

2. Haki ya makao ya Familia (matrimonial home).

Matrimonial home imefafanuliwa chini ya kifungu cha 2(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971, kama Eneo ambapo wanandoa wanaishi. Kutokana na hali ilivyosasa ambapo kuishi pamoja chini ya paa moja kwa wanandoa sio lazima. Ili kujua makao ya familia mambo yafuatayo yataangaliwa;

  • Watoto wanapoishi
  • Ni wapi wanandoa wameamua kuwa makao yao.
  • IKUMBUKWE: Makao ya familia(Matrimonial home) si lazima iwe nyumba wanayomiliki wanandoa, wanaweza kuwa wamepanga. Lakini matrimonial house(Nyumba ya wanandoa) ni ile inayomilikiwa na wanandoa wenyewe.
  • Kifungu cha 59(1) cha sheria ya Ndoa ya 1971 kinaeleza kuhusu ulinzi wa mali za Ndoa ikiwemo nyumba, inazuingua mwanandoa mmoja kuuza ama kuweka bond mali zilizopatikana kwa juhudi za pamoja za wanandoa wote, bila ridhaa ya Mwanandoa mwingine. Kama mwanandoa mmoja atauza bila ridhaa ya mwingine, basi ambaye hajaridhia ana haki ya kukaa kwenye nyumba hiyo mpaka ndoa itakapovunjwa au mahakama itakapotoa amri ya kutengana.

Katika kesi ya Leonce Chalamila v. Masala Edward Masunga[1999] HC CA 150.

“Mjibu maombi alinunua kipande cha  ardhi kilichopo Mji mwema kurasini mwaka kutoka kwa bwana Mategetwa 1992, baada ya kununua ardhi hiyo alianza ujenzi wa nyumba lakini kabla ya kumaliza, alikutwa na kesi ya jinai na kufungwa miezi 9 jela, wakati akiwa gerezani mke wake Esther aliuza kiwanja na nyumba kwa Tshs. 500,000/= na kurudi kwao Tabora. Mumewe alipomaliza kifungo chake alishangazwa kukuta nyumba yake imebomolewa na imejengwa nyumba mpya katika kiwanja chake. Mume alifungua kesi mahakamani ambapo mahakama iliamuru mnunuzi mpya kuondoka mara moja katika eneo hilo, kwa sababu mke hakuwa na uwezo wa kuuza nyumba bila ridhaa ya mume.”

3. Haki ya kumiliki Mali.

Sheria ya Ndoa ya 1971 chini ya kifungu cha 56 inatoa fursa sawa kwa mwanaume na mwanamke ambao ni wanandoa kutafuta, kumiliki mali kwa pamoja na kwa mmoja mmoja(separate ownership of property) kifungu cha 58. Zile mali zilipokuwa zikimilikiwa na mwanandoa kabla ya ndoa si mali za wanandoa, lakini vilevile hata baada ya kuingia kwenye ndoa wanandoa wana haki ya kumiliki mao zao binafsi kila mmoja tofauti na mali za ndoa.

4. Haki na wajibu chini ya sheria ya makosa ya jinai.

Kila mwanandoa atawajibika kwa kosa lake mwenyewe, mume au mke hawezi kushtakiwa au kuwajibikia makosa ya mwingine. Yaani Mke akifanya kosa la jinai, hauwezi kumshtaki mke kwa kosa hilo. Na hata wanandoa wenyewe wanaweza kushtakiana wao kwa wao kwa makosa ya jinai. Mfano mume akimuibia mke mali yake, Mke anaweza kumshtaki mume kwa kosa hilo.

5. Haki na wajibu katika sheria za mikataba.

Miaka ya nyuma mke na mume walikuwa hawawezi kuingia mkataba, lakini sasa Mke na mume wanaweza kuingia mkataba miongoni mwao. Sharti la lazima tu ni kwamba LAZIMA WAONYESHE NIA YA KUANZISHA MAHUSIANO YA KISHERIA na NI LAZIMA IWE MAKUBALIANO YA KIBIASHARA. Aidha wanandoa wanaweza kuingia mkataba na mtu mwingine.

6. Haki na wajibu katika sheria ya tindi(Tort).

Msimamo wa sheria ulivyo kwa sasa ni kuwa mke au mume, anaweza kushtaki au kushtakiwa kivyake(separately) katika sheria za tindi(tort) isipokuwa kwa kifungu cha 56 kuhusu haki za kimkataba. Kipindi cha nyuma wanawake au mke hakuweza kushtaki au kushtakiwa katika tort bali Mume alichukua nafasi katika hilo. Kifungu cha 65 kinakataza Mume kuwajibika kwa niaba ya mke kwa makosa ya tort. Vile vile mke na mume wanaweza kushtakiana wao kwa wao kwa makosa ya tort. Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kwamba Mke au mume hawezi kushtaki kwa ajili ya fidia inayotokana na kitendo cha uzembe or kutotekeleza wajibu kwa kukosa Consortium kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 65 (c).

7. Haki na wajibu wa wanandoa katika sheria ya ushahidi.

Katika Sheria ya Ushahidi ya Tanzania (Evidence Act, Cap. 6 R.E 2022), haki na wajibu wa wanandoa kuhusu ushahidi zinahusu masuala kama ushahidi wa ndoa, ushahidi wa siri za ndoa, na uwezo wa mmoja kumshuhudia mwenzake. Hizi ni baadhi ya haki na wajibu muhimu:

Haki za Wanandoa katika Ushahidi

(i) Haki ya Kutotoa Ushahidi Dhidi ya Mwenzake

Kifungu cha 130(1) cha Sheria ya Ushahidi kinasema kuwa mke au mume hawezi kulazimishwa kutoa ushahidi dhidi ya mwenzake katika kesi ya jinai, isipokuwa katika mazingira maalum.


(ii) Haki ya Kulindwa Siri za Ndoa

Kifungu cha 131 kinalinda mawasiliano ya siri kati ya wanandoa. Hii ina maana kuwa mmoja hawezi kufichua mambo ya faragha aliyoyapata kutoka kwa mwenzake wakati wa ndoa, hata kama ndoa imevunjika.


(iii) Haki ya Kutoa Ushahidi kwa Hiari

Ingawa wanandoa hawawezi kulazimishwa kushuhudia dhidi ya wenzao, wanaweza kutoa ushahidi kwa hiari katika baadhi ya kesi, hususan zile zinazohusu uhalifu dhidi yao au watoto wao.

Wajibu wa Wanandoa katika Ushahidi

(i) Wajibu wa Kutoa Ushahidi kwa Maslahi ya Haki

Katika kesi zinazohusu madhara kwa watoto wao au jinai kama unyanyasaji wa kijinsia, mmoja anaweza kuwa shahidi dhidi ya mwenzake.

(ii) Wajibu wa Kuhifadhi Siri za Ndoa

Mwanandoa hawezi kufichua mawasiliano ya faragha kati yake na mwenzake, hata baada ya ndoa kuvunjika, isipokuwa pale sheria inapohitaji.

(iii) Wajibu wa Kushuhudia Katika Kesi Maalum

Ikiwa mmoja wa wanandoa anashitakiwa kwa kosa lililofanywa dhidi ya mwenzake, kama vile unyanyasaji wa mwili, mke au mume anaweza kutoa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa.

Kwa ujumla Sheria ya Ushahidi inatoa ulinzi kwa wanandoa kwa kuhakikisha kuwa hawalazimishwi kushuhudia dhidi ya wenzao, lakini pia inaweka wajibu wa kutoa ushahidi katika kesi zinazohusu uhalifu mkubwa kama vile unyanyasaji wa watoto au mume/mke. Haki na wajibu hivi vinalenga kulinda ndoa lakini pia kuhakikisha haki inatendeka.

8. Usawa miongoni mwa wake.

Kwa wale wanaooa mke zaidi ya mmoja kwa mfano waislamu sheria  ya Ndoa chini ya kifungu cha 57 inataka kuwe na usawa katika wake wote pasipo upendeleo wowote. Aidha kifungu cha 66 cha sheria hiyohiyo kimezuia adhabu ya viboko kwa mwanandoa na aina yoyote ya ukatili.

9. Haki na wajibu kuhusu watoto.

Ni vizuri kutambua kuwa watoto ni watoto, wawe wamezaliwa ndani ya ndoa au walipatikana nje ya ndoa ustawi wa mtoto unabaki kuwa kipaumbele cha juu zaidi. Kifungu cha 7 cha sheria ya Ndoa ya 1971 kinasisitiza kuwa mtoto anapaswa kuishi na wazazi wake au walezi wake,na hakuna anayetakiwa kupora haki hii kutoka kwa mtoto. Na wazazi au walezi wana wajibu wa kumlea mtoto katika mazingira salama na tulivu. Inawezekana mtoto asiishi na wazazi wake hata kama wako hai, na hii ni iwapo tu kama akiishi na wazazi wake itaharibu ustawi wake au atapata mateso.

Kifungu cha 129(1) cha Sheria ya mtoto kinataka Wazazi wote wawili iwe wanaishi na mtoto au hapana, wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anapata ustawi mzuri na uangalizi. Aidha kifungu cha 129(2) kinaweka wajibu kwa mwanamke kuwatunza na kuwaangalia watoto, ikiwa baba amefariki au taarifa zake hazijulikani au hana uwezo wa kuwatunza.

9. Makazi ya watoto baada ya wazazi kutengana au kuachana.

Miongoni mwana dhana maarufu sana ni ile ya kwamba pale wazazi wanapotengana au kuachana, mtoto chini ya miaka 7 ataishi na mama yake, mapaka atakapofikia umri wa miaka 7 kifungu cha 125(3) na 126(2). Hata hivyo ni muhimu kutambua kuwa kigezo kikubwa kinachozingatiwa, wakati wa kutoa amri ya mtoto akae na nani ni maslahi mapana ya mtoto, kama ilivyoelezwa katika sheria ya mtoto kifungu cha 39(1) na (2). Maoni ya mtoto mwenyewe kama yatatolewa huru yamapaswa kusikilizwa.

Kwa hivyo katika kuamua mtoto ataishi na nani ni muhimu sana kuzingatia Ustawi wa mtoto, Matakwa za wazazi wa mtoto, maoni ya Mtoto mwenyewe ambayo lazima yatolewe kwa uhuru bila shinikizo na mwisho ni Mila na desturi ya jamii wanakotoka wazazi(kifungu cha 125(2) cha sheria ya Ndoa).

Maamuzi ya mtoto ataishi na nani yanaweza kufanywa na familia, Jamii au wakishindwa Mahakama.

HAKI ZA KUCHUKUA HATUA ZA KINDOA(MATRIMONIAL RIGHT OF ACTION.

  1. Haki ya fidia kwa kuvunja ahadi ya kuoa/kuolewa. Kifungu cha 69(1) na 70 cha sheria ya Ndoa.
  2. Haki ya kurudishiwa zawadi zilizotolewa kwa ahadi ya ndoa, kifungu cha 71 kinatoa haki ya kuomba kurudishiwa zawadi zile tu zilitolewa kwa nia ya kuja kufunga ndoa, na lazima pande zote ziwe zilielewa kuwa zawadi hizi ni kwa ajili ya kufunga ndoa baadae.
  3. Haki ya kulipwa fidia kwa fumanizi/Uzinzi(adultery). Kifungu cha 72(1) cha sheria ya Ndoa kinatoa haki kwa upande wowote wa wanandoa kushtaki mtu yeyote atakaye fumaniwa na mke/Mume wa upande mwingine na kulipwa fidia. Hata hivyo kesi hiyo haiwezi kufanikiwa iwapo MOJA, Mlalamikaji aliridhia mke/mume afanye kitendo hicho na MBILI, Ikiwa fidia hiyo itadaiwa katika maombi ya talaka.
  4. Maombi ya fidia ya fumanizi/uzinzi na mke au Mume wa mtu yanaweza kufutwa, iwapo mahakama itajiridhisha kuwa aliyefuminiwa hakujua, na asingeweza kujua kwa namna yeyote ile iliyo thabiti kuwa mtu aliyefumaniwa naye alikuwa ameoa au kuolewa. Hili limeelezwa katika kifungu cha 72(2) cha sheria ya Ndoa.

NATUMAINI UMEELIMIKA USIKOSE KUFUATILIA MAKALA NYINGINE YA SEHEMU YA PILI, ITAKAYO JADILI MASHTAKA YA KINDOA NA VYOMBO VYENYE MAMLAKA YA KUSHUGHULIKA NAYO.


Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Published by LEGALJAMIIโš–๏ธ

Richard Kalokola is a Tanzanian legal professional with a Bachelor of Laws (LL.B) from St. Augustine University of Tanzania and professional training from the Law School of Tanzania. He has a strong passion for legal education, research, and public legal awareness. As the founder of LegalJamii, Richard is dedicated to bridging the gap between complex legal principles and everyday understanding by delivering accurate, practical, and accessible legal information. His vision is to promote a legally informed society where individuals, businesses, and communities can confidently understand their rights, responsibilities, and available legal solutions. Through LegalJamii, he continues to advance legal literacy by transforming legal concepts into clear and simplified language for the benefit of the wider public.

Leave a Reply

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading