
Ni hatua mojawapo katika kesi za jinai ambapo mtuhumiwa ama mshukiwa huachiwa na mahakama au polisi Kwa masharti Fulani, Kwa lengo la kuihakikishia mahakama au jeshi la polisi kuwa atakuwepo pindi atakapohitajika na mamlaka hizo. Dhamana ni kuachiliwa Kwa Muda Kwa mtuhumiwa wakati kesi ikiendelea mahakamani au upelelezi ukiendelea Polisi. Dhamana inatokana na dhana maarufu kisheria ifahamikayo kama DHAHANIO LA KUTOKUWA NA HATIA yaani (Presumption of Innocence) yenye maana Kwamba Kila mtu atachukuliwa kuwa hana hatia mpaka itakapothibitika mahakamani.
Aina za Dhamana.
Dhamana zipo za aina mbili, Dhamana inayotolewa na Polisi na Ile inayotolewa na mahakama. Kifungu cha 148 cha Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kimeeleza Kwa kina. Hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa sio Kila kosa linaweza kutolewa dhamana. Yako makosa yasiyodhaminika kutokana na ukubwa wake mfano Mauaji, uhaini, uporaji kwa kutumia silaha n.k, vile vile zipo sababu Fulani zinazoweza kufanya mtuhumiwa asipatiwe dhamana hata kama kosa linadhaminika. Dhamana pia huendana na masharti yenye Lengo la kuihakikishia mamlaka husika inayotoa dhamana (polisi au mahakama) Kwamba mtuhumiwa atakuwepo atakapo hitajika. Masharti hayo ni kama kuwa na Wadhamini wakaazi na wenye vitambulisho vya uraia, kuweka mali ama Bondi na Kwa barua ya utambilisho. Kwa upande wa dhamana inayotolewa na mahakama imegawanyika kutokana na hatua ya kesi husika. Zipo Dhamana wakati shauri likiendelea mahakamani(Bail pending trial), Dhamana wakati Shauri la Rufaa likiendelea(Bail pending Appeal) na dhamana wakati wa uchunguzi wa kesi kabla ya kupelekwa Mahakama kuu (Bail during Committal Proceedings)
Dhamana wakati shauri la msingi likiendelea mahakamani yaani Bail pending trial Huwa ni haki Kwa mtuhumiwa, hii inatokana na ukweli Kwamba katika hatua hii ya kesi Bado mahakama haijathibisha iwapo mtu yule mbele yake ana hatia au la,ndiyo maana anaitwa MTUHUMIWA Kwa hivyo upo uwezekano wa kukutwa hana hatia ndio maana dhamana inakuwa haki yake chini ya dhana Ile niliyoeleza mwanzo ya Dhahanio la KUTOKUWA na hatia (Presumption of Innocence). Ni uonevu mbele ya macho ya Sheria kumnyima mtu dhamana bila sababu ya msingi. Kwa upande Mwingine Dhamana wakati shauri la Rufaa likiendelea (Bail pending Appeal) hii si haki bali ni aina Fulani ya upendeleo tu. Kwa sababu tayari mtu yule si mtuhumiwa tena anakuwa ameshathibitishwa na Mahakama kuwa anayo hatia. Hivyo Dhahanio la KUTOKUWA na hatia haliwezi kufanya kazi kwake kutokana na kutiwa hatiani na mahakama (convicted person) hivyo aina hii ya dhamana huchukuliwa kama upendeleo na si haki, na huendana na masharti makali ikiwemo lazima mwombaji awe ana nafasi kubwa ya kushinda Rufaa yake .
Ni muda Gani sahihi kuomba dhamana ukiwa mahakamani. Na inaombwaje?
Dhamana inapaswa kuombwa katika hatua za awali kabisa za shauri yaani mara baada ya mtuhumiwa kusomewa mashtaka yake na akayajibu(kweli au Sikweli) anapaswa kuomba dhamana yeye mwenyewe au kuombewa na wakili wake kama yupo. Na mara nyingi huombwa Kwa mdomo tu bila ya ulazima wa kuwa na nyaraka za maombi kama shauri lipo Mahakama za chini ya Mahakama kuu.(Subordinate courts). Lakini Kwa Mahakama kuu dhamana inaweza kuombwa Kwa kutumia nyaraka maalumu za maombi (Chamber Summons) inayoambatana na hati ya kiapo (affidavit)
Hata hivyo sio lazima kuomba dhamana katika wakati huo niliouainisha hapo juu, inawezekana Mtuhumiwa hakuwa na wakili wakati huo na hakufahamu kuhusu haki ya dhamana, hivyo baadaye shauri likiwa linasikilizwa akapata wakili na kuhitaji dhamana Bado anayo nafasi ya kuiomba. Wakili wake anaweza kwenda Mahakamani mbele ya hakimu husika na kumuomba Kwa barua rasmi au mdomo atoe Amri ya kumleta mtuhumiwa Mahakamani (Removal order) katika tarehe na muda utakao tajwa na Amri hiyo na upande wa pili wanapaswa kutaarifiwa Kwa ajili ya kuja kwa usikilizwaji wa maombi ya dhamana. Kwani upo uwezekano wa upande wa pili kuwa na mapingamizi dhidi ya Maombi hayo ya Dhamana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo:-
1.Kwamba mtuhumiwa akiachiwa ataingilia uchunguzi.
2. Kwamba anayorekodi ya kutoroka mara baada ya kupewa dhamana katika makosa mengine huko nyuma.
3. Kwamba ni kweli kosa lake linadhaminika lakini usalama wake katika jamii uko hatarini iwapo ataachiwa.
4. Kwamba amesababisha majeraha makubwa Kwa mtu ambaye Yuko hospitali na Hali yake ni mbaya katika kiwango ambacho Kuna wasiwasi mtu yule anaweza kufariki na kosa kubadilika kuwa Mauaji.
5. Kwamba kumuachia mtu huyu Kwa dhamana ni tishio la usalama wa jamii anakotoka.
Na sababu nyingine nyingi kutokana na mazingira ya shauri husika.
Dhamana wakati wa uchunguzi wa kesi katika Mahakama za chini ya Mahakama kuu. Bail during Committal Proceedings. Katika hatua hii lazima kuelewa kuwa hii hutokea katika makosa yote ambayo hupaswa kusikilizwa na Mahakama kuu pekee, lakini kabla ya kufikishwa Mahakama kuu ni lazima uchunguzi na upelelezi ukakamilika na kuwa na jarada la kesi lililokamilika ndipo hupatishwa Mahakama kuu. Kwa tafsiri rahisi ni Kwamba Mahakama za chini husaidia tu kukamilisha uchunguzi ila hazina mamlaka ya kusikilizwa kesi za aina hii. Mamlaka ya kusikilizwa kesi hizo Huwa ni ya Mahakama kuu pekee. Mfano wa makosa hayo ni kama Mauaji na Makosa ya uhujumu Uchumi yaani Economic crimes.
Ni Mahakama Gani sahihi kuomba dhamana katika mazingira tajwa hapo juu hususani Makosa ya kiuchumi?
1. Kama shauri Kwa ajili ya uchunguzi Bado lipo katika Mahakama ya chini (Subordinate court) na thamani ya kosa alilofanya halizidi shilingi milioni 300. Dhamana itaombewa palepale kwenye Mahakama ya chini ya Mahakama kuu
2. Kama shauri limeshafika Katika Mahakama kuu Divisheni ya rushwa na uhujumu Uchumi na thamani ya kosa alilofanya ni zaidi ya Shilingi milioni 300. Dhamana itatolewa na Mahakama kuu Divisheni ya Rushwa na uhujumu Uchumi.
3. Kama shauri Bado halijaanza katika Mahakama kuu Divisheni ya rushwa na uhujumu Uchumi na thamani ya kosa tendwa ni zaidi ya milioni 300. Dhamana itatolewa na Mahakama kuu ya kawaida. (Ordinary High Court)
4. Kama shauri lipo kwenye Mahakama ya chini lakini thamani ya kosa lililofanywa haijajulikana Bado. Dhamana itatolewa na Mahakama kuu ya kawaida. (Ordinary High Court)
Andiko na Richard Kalokola.
kalokolarichard1@gmail.com
Discover more from 𝐋𝐄𝐆𝐀𝐋𝐉𝐀𝐌𝐈𝐈⚖️
Subscribe to get the latest posts sent to your email.


Nimejifunza Jambo