HISTORIA YA KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MABADILIKO YAKE MBALIMBALI.

Kwa tafsiri nzuri na itakayoeleweka Zaidi “KATIBA” Ni Sheria mama ama Sheria kuu iwe katika Nchi ama taasisi Fulani. Katiba katika Muktadha wa Nchi Ni Sheria mama ambayo huweka misingi mikuu ya kisheria katika Nchi. Katiba huweka miongozo ambayo hufafanuliwa Zaidi katika Sheria nyingine zitakazotungwa na Bunge ama zitakazotungwa Kwa utaratibu mwingine ulioelekezwa na Bunge.

Kwanini Sheria Mama?

Dhana ya Katiba kuitwa Sheria Mama ina chimbuko lake kutoka ibara za 63(3) (d) na 64 ibara ndogo ya 1 Hadi ya 5 ya Katiba ya Mwaka 1977 ambayo Kwa ujumla wake inatoa mamlaka Kwa Bunge kutunga Sheria Kwa Mambo ya muungano na Tanzania bara, na Baraza la wawakilishi Kwa Mambo ya Tanzania Zanzibar. Aidha ibara ndogo ya 5 ya ibara ya 64 imeeleza kuwa Katiba hii itakuwa na nguvu katika eneo lote la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Sheria yoyote itakayokinzana au itakayopingana na ibara za Katiba hii

Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Kama ilivyofanyiwa marekebisho 2005 ndio Katiba tiliyonayo sasa, na ambayo ilianza kufanya Kazi tarehe 26/04/1977. Tangu Mwaka 1977 Hadi sasa Katiba hii imefanyiwa marekebisho mara Kumi na nne (14) kupitia Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kati ya Agosti 1979 Hadi April 2005.

HISTORIA YA KATIBA.

Historia ya Katiba ya Tanzania na mchakato wa kuundwa kwake unaweza kuangaziwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1920 na 1961 wakati Tanganyika ilipopata UHURU wake. Kabla ya Mwaka 1961 Tanganyika ilitawaliwa wa wakoloni wa Kijerumani (1885-1918) na Waingereza (1919-1961). Wakoloni wa kiingereza walikuwa na mchango mkubwa sana katika kuibua muundo na mfumo wa Katiba. Kwani hata Jina “Tanganyika” Ni matokeo ya utawala wa kikoloni wa kiingereza kupitia Nyaraka iliyopewa Jina la THE TANGANYIKA (CONSTITUTION) ORDER IN COUNCIL ya Julai 1920.

THE TANGANYIKA ORDER IN COUNCIL 1920.

Nyaraka hii chini ya utawala wa Waingereza inachukuliwa kuwa ndio iliyoweka msingi wa historia na muundo wa Katiba ya Tanzania. Nyaraka hii kuu pamoja na Mambo mengine lakini ndiyo iliyoanzisha eneo tawala la Tanganyika (territory of Tanganyika) , Baraza la kibunge la kutunga Sheria la Tanganyika (Legislative Council) na Muundo wa kimahakama. Kwa ujumla TOC ya 1920 inachikuliwa Kuwa mwanzo wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mfano mambo kama Mahakama Kuu ya Tanganyika ilitamkwa na kuanzishwa rasmi chini ya ibara ya 17(1) ya TOC, 1920. Aidha Common Law, doctrine of Equity na Statutes of General Application pia zilitumika chini ya nyaraka hii kufuatana na mazingira ya kipindi hicho.

Mbali na TOC ya 1920, Muendelezo wa mabadiliko ya Katiba ulijenjwa pia katika utungwaji wa Sheria iliyoitwa Tanganyika(Legislative Council) Order in Council, 1926 ambayo ilichochea utendaji wa Baraza la kutunga Sheria ndani ya Tanganyika. Hata hivyo ikumbukwe kulikuwa na matoleo mbalimbali ya hizi TOC hadi ile ya 1961 yaani Tanganyika (Constitution) Order in Council, 1961 ambayo iliziondoa TOC nyingine zote za awali na ilikuwa maalumu Kwa ajili kuitangaza rasmi Katiba ya Tanganyika na uhuru wake ndani ya Jumuiya ya Madola.

KATIBA YA UHURU YA TANGANYIKA, 1961.

Itakumbukwa Tanganyika ilipata uhuru wake Disemba 9, 1961, kupatikana Kwa uhuru wa Tanganyika kulililazimisha Bunge la wingereza kutunga Sheria ya uhuru wa Tanganyika (The Tanganyika Independence Act,1961) ambayo ililenga kuitambua Tanganyika Kuwa nchi huru ndani ya Jumuiya ya Madola.

Mchakato wa kutungwa Kwa Katiba ya uhuru ya Tanganyika ulifanywa na Wingereza na serikali ya Tanganyika chini ya mwamvuli wa TANU jijini Dar es Salaam. TANU iliandaa mkutano wa Katiba ulifanyika Karimjee Hall tarehe 27/03/1961 ili kuwezesha ushiriki wa Umma na kupata maoni yao. Mkutano ule ulikuja na Rasimu ya mapendekezo ambayo ilijumuisha Kuwa Tanganyika inapaswa Kuwa Jamuhuri na TANU iliondoa Mswada wa haki za binadamu na kukataa usijumuishwe kwenye Katiba. Hata hivi utunzi wa kibunge wa Katiba hii ya Uhuru uliendeshwa na Wingereza Kwa kutumia waandishi wa Sheria wa kiingereza (English draftsmen). Katiba hii ilitumia Muundo wa kiutawala wa Westminster ambapo kunakuwa kiongozi wa Nchi (Malkia wa Wingereza kipindi hicho) halafu na kiongozi wa Serikali (Waziri Mkuu) ambaye alikuwa Mwalimu J.K. Nyerere. Hii ndiyo sababu baada ya kupata Uhuru Tanganyika Mwaka 1961 haikuwa na Rais Bali Waziri Mkuu. Na Malkia wa Wingereza aliwakilishwa na Gavana wa Tanganyika. Kwa ujumla Katiba ya Tanganyika wakati wa uhuru ilikuwa Mwangaza wa kutamatisha kipindi kirefu cha ukoloni na kuanza enzi Mpya ya Uhuru ingawa dhana ya kijitawala kikamilifu ilikuwa bado.

KATIBA YA JAMUHURI YA TANGANYIKA YA MWAKA 1962.

Itakumbukwa Kuwa katika mkutano wake wa Katiba wa tarehe 27/03/1961 TANU pendekeza na kuomba Tanganyika Kuwa Jamuhuri haraka iwezekanavyo, hata hivyo mapendekezo hayo yalipuuzwa na Wingereza Kwa Muda Fulani, hata hivyo tarehe 15/02/1962 Bunge lilitakiwa kujadili mabadiliko yatakayohitajika ili kuifanya Tanganyika Kuwa Jamuhuri. Kiu ya Tanganyika Kuwa Jamuhuri ilitokana na mambo makubwa matatu:-

1. Katiba ya Uhuru ya 1961 ilikuwa imeunganishwa na utawala wa Kifalme.

2. Katiba ya Uhuru ya 1961 haikutokana na mawazo ya Watu wa Tanganyika.

3. Ilitungiwa Wingereza na kupitishwa kwenye Bunge la Wingereza kama Sheria ya kawaida ya Wingereza na ilikuwa Kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya Wingereza nchini Tanganyika.

Mnamo Disemba 9, 1962 Tanganyika ilitangazwa rasmi Kuwa Jamuhuri kupia Sheria ya Bunge la Wingereza (Tanganyika Republic Act, 1962) Katiba hii ya Jamuhuri iliondoa Mamlaka ya Malkia na utawala wa Kifalme katika uendeshaji wa Tanganyika. Mara baada ya Sheria hiyo ya Mwaka 1962, Sheria ya Bunge Maalumu la Katiba (Constituent Assembly Act, 1962) ilitungiwa na Tanganyika Kwa ajili ya kuanza mchakato wa kutunga katiba ya Jamuhuri.

Mchakato wa kutunga katiba ya Jamuhuri ulikuwa wa kushangaza kidogo Kwa sababu mnamo 22/11/1962 Bunge la Tanganyika kupitia Sheria ya Bunge Maalumu la Katiba lilijigeuza lenyewe Kuwa Bunge Maalumu la Katiba Bila mabadiliko yoyote ya kimuundo, na Kwa kubwa isivyokuwa kawaida siku Moja baadae yaani tarehe 23/11/1962 Katiba ya Tanganyika ya Jamuhuri ilitungwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali, Vol.XLIII, No. 65/dated 7th December, 1962. Kwa lugha nyingine Katiba ya Jamuhuri ya Mwaka 1962 ilitungwa na Bunge la Tanganyika na si Bunge Maalumu la Katiba.

Katika hili ni Muhimu kukumbuka Kwamba Bunge Kwa kipindi hicho lilikuwa linaundwa na wajumbe 71 , ambapo 70 Kati ya Hao walikuwa ni kutoka TANU na mmoja aliyesalia alikuwa Mgombea binafsi. Kwa hiyo Katiba ya Jamuhuri ya Tanganyika ya Mwaka 1962 ndio ilikuwa Katiba ya pili ya Tanganyika baada ya Ile ya Uhuru na ndio ilikuwa msingi wa Katiba zilizotengenezwa na wazawa, hii ni kutokana na

1. Kujuisha watu wa Tanganyika katika mchakato wa utunzi wake.

2. Ni utaratibu jumuishi wa uridhiaji wake.

Ujio wa Katiba hii ya Jamuhuri uliundwa mamlaka ya Rais Kwa namna tatu ambapo:

(a) Nguvu kubwa za kiutawala zilivishwa Kwa Rais wa Jamuhuri.

(b) Rais alipewa mamlaka ya kuwa Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali, na Amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

(C) Rais alifanywa kuwa Sehemu ya Bunge.

KATIBA YA MPITO YA JAMUHURI YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR, 1964.

Kama ilivyoelezwa hapo awali mabadiliko ya Katiba huweza kuchochewa na mabadiliko na uhitaji na uhitaji wa jamii Kwa wakati huo. Katiba hii ya mpito ilikuja ili kujumuisha kwenye Katiba tukio la Muungano wa katika ya Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar mnamo Mwaka 1964. Muungano huu uliasisiwa na viongozi wasisi wa Nchi hizo Mbili Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume mnamo tarehe 26/04/1964 na kufuatia na kusainiwa Kwa hati za Muungano pale Karimjee Hall tarehe 27/04/1964, Jambo hili lililazimisha mabadiliko ya Katiba ya Jamuhuri ili kuweka ibara zinazozungumzia Muungano. Sheria mahususi ya Muungano ilitungwa na Bunge na ilijulikana kama the Union of Tanganyika and Zanzibar Act No 22 of 1964, na Kwa upande wa Zanzibar hati za Muungano ziliingizwa kwenye Sheria iliyojulikana kama Union of Zanzibar and Tanganyika Law of 1964. Mabadiliko haya ya Katiba yalifanywa kupitia Decree ya Rais iliyoitwa Interim Constitutional decree of 1964

Kuundwa Kwa Jina Jipya la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kubadili Jina kutoka Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar kwenda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ulikuwa ni mchakato uliochukua Muda kiasi, historia inaonyesha kuwa mnamo tarehe 31/07/1964 Umma ulialikwa kupendekeza Jina Jipya baada ya Muungano. Takribani majina 677 yalipendekezwa na Umma, na hatimaye Jina Tanzania lilikubaliwa na Serikali. Na sababu za kukubalika Kwa Jina hili ilikuwa ni mjumuisho wa herufi Mbili za mwanzo kutoka kila Nchi ambazo ni Tan na Za na hivyo kuonekana kuwa ni Jina linalobaki kuwa alama ya Muungano.

KATIBA YA MPITO YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 1965.

Hii ni Katiba ambayo ililenga kutambulisha mfumo wa Chama kimoja ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba hii haikujumuisha Bunge maalumu la Katiba. Muswada wa mabadiliko haya ulitungwa Julai, 1965 and kuwasilishwa Mbele ya Bunge, na Bunge Kwa kutumia mamlaka ya kawaida ya kibunge ilipitisha Sheria No. 43 ya Mwaka 1965. Kwa Lugha nyingine Katiba hii ilipitishwa na Bunge kama Sheria ya kawaida ambayo hutungwa na Bunge. Katiba hii ilianza Kazi tarehe 11/07/1965 na ilikuwa na jumla ya Sura 9 na Majedwali mawili, Ambapo jedwali la Kwanza ilikuwa ni Katiba ya TANU na Sura ya Kwanza ilianzisha mfumo wa Chama kimoja cha Siasa ambapo Kwa wakati huo ilikuwa TANU.

Kutokana na uundwaji wake na kuambatanishwa Kwa Katiba ya TANU kama Sehemu ya Katiba hiyo ilikuwa Ngumu kutenganisha na kujua iwapo ilikuwa ni Kwa ajili ya maslahi ya watu wa Tanzania Kwa ujumla au maslahi ya Wanatanu. Katiba hii ya Muda ilidumu Kwa miaka 12 ilifanyiwa mabadiliko mara 13 mpaka kufukia Julai, 1975.

KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 1977.

Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, na marekebisho yake Mbalimbali ndio Katiba ya Sasa na inayofanya Kazi ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wengine wengi hupenda kuiita Katiba ya Kudumu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa Mimi napingana na mtazamo huo Kwa sababu Sheria yoyote ikiwemo Katiba ina sifa ya kubadilika kulingana na Wakati na mahitaji kama tulivyoona hapo juu namna ambavyo mahitaji yalipelekea mabadiliko Mbalimbali. Katiba hii ya Mwaka 1977 ilikuja kama matokeo ya kuungana Kwa Chama cha TANU na ASP na kuundwa Kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 05/02/1977. Baada ya Muungano huo Chama hicho kipya kiliendelea na jitihada za kupatikana Kwa Katiba ya Kudumu Kwa kuunda Tume ya Katiba tarehe 16/03/1977, uundwaji huu wa Tume ulitangazwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kupitia GN. NO. 38 la tarehe 25/03/1977, katika tarehe hiyo hiyo pia Rais aliunda na kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu Kwa Kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba hiyo.

Tume hiyo ya Katiba iliundwa na wajumbe 20 Ambapo 10 walitokea Tanzania Bara na 10 wengine kutoka Zanzibar. Tume hii iliundwa na wajumbe ambao walikuwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi na iliongozwa na BW. THABIT KOMBO. Hata hivyo wanahistoria wanaeleza Kwamba Tume hiyo ya Katiba ilianza Kazi Mapema hata kabla ya uteuzi rasmi. Tume hii ndani ya kipindi cha Muda mfupi sana iliandaa Rasimu ya Katiba na kuiwasilisha Mbele ya Halmashauri Kuu ya CCM, na NEC ikachambua Katiba pendekezwa hiyo Bila kuhusisha Umma na katika kikao cha siku Moja tu Halmashauri Kuu ya CCM iliridhia Rasimu hiyo. Katiba hiyo Pendekezwa ilihanishwa kwenye mfumo wa Muswada, ambao ulichapishwa mnamo 18/04/1977 na ndani ya siku Saba uliwasilishwa kwenye Bunge la Katiba ambalo lilikutana tarehe 25/04/1977

Kwa Upande Mwingine Bunge la Katiba liliundwa na wajumbe 207, Ambapo wajumbe 45 walitokea Zanzibar, Kwa uhakika kabisa wabunge wa wakati huo ambao wengi walitokana na TANU ndio haohao waliounda Bunge maalumu la Katiba, ingawa utaratibu wa kikatiba unataka Vyombo hivi kuwa viwili tofauti na kufanya Kazi Kwa namna tofauti. Katiba hii ya Mwaka 1977 ilianza kutumika Rasmi tarehe 27/04/1977.

Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 iliingiza marekebisho katika Makundi makubwa mawili:-

1. Marekebisho Maalumu yaliyojumuisha pamoja na mambo mengine orodha ya mambo ya Muungano, Uwepo wa Jamuhuri ya Muungano, Mamlaka ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar ambayo ilihitaji akidi ya theluthi Mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na akidi ya  theluthi Mbili pia kutoka Zanzibar.

2. Marekebisho ya Jumla katika ibara nyingine za Katiba yaliyohitaji akidi ya theluthi Mbili ya wabunge wote ndani ya Bunge.

Mpaka Sasa Katiba hii ina miaka 47 Tangu Mwaka 1977 na kutokana na ukweli kuwa mambo mengi yamebadilika na katikati mwa miaka ya 2005 Hadi 2010 kulianza kuwa na vuguvugu la madai ya Katiba mpya, na ndipo Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete iliamua kuanzisha mchakato na kutunga Katiba Mpya.

Wakati huu mchakato ulianza Kwa kutunga Sheria ya mabadiliko ya Katiba na kufuatiwa na uundwaji wa Tume ya kukusanya maoni kutoka katika mabaraza ya Mbalimbali ya Katiba katika ngazi Mbalimbali, baada ya hapo Tume ilikabidhi Rasimu ya Kwanza ya katiba na kuiwasilisha Mbele ya Bunge maalumu Kwa ajili ya kupitia na kufanya marekebisho, baada ya hapo, Bunge maalumu lilikuja na Rasimu ya Pili ya Katiba mnamo Mwaka 2014, ambayo ni maarufu kama Katiba inayopendekezwa. Mchakato uliobaki ilikuwa ni kura ya Maoni Kwa wananchi wa Tanzania ili kujua iwapo wanaikubali ili ipitishwe na kuwa Katiba kamili.

Tofauti na awamu nyingine zote za kutunga Katiba, Mchakato wa Mwaka 2014 ilikuwa Bora Kwa sababu ulizingatia Zaidi suala la ushirikishwaji wa wananchi katika Makundi Mbalimbali, kuanzia kwenye ukusanyaji wa Maoni Hadi kwenye uwakikishi katika Bunge maalumu la Katiba Ambapo kulikuwa na wajumbe 201 walioteuliwa kutoka Makundi Mbalimbali, na asasi Mbalimbali za kiraia na kijamii.

Hitimisho

Kwa Sasa bado madai ya kuendeleza na kumalizia mchakato uliokwama Mwaka 2014 yameanza kuibuka Tena kupitia taasisi Mbalimbali na Serikali ilieleza utayari wake katika kufufua mchakato huo Ambapo bado mpaka Sasa tarehe 19/04/2024 utaratibu wa namna ya kufufua mchakato huo haujaanza.

Na Richard Kalokola.@richardkalokola


Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Published by LEGALJAMIIโš–๏ธ

Richard Kalokola is a Tanzanian legal professional with a Bachelor of Laws (LL.B) from St. Augustine University of Tanzania and professional training from the Law School of Tanzania. He has a strong passion for legal education, research, and public legal awareness. As the founder of LegalJamii, Richard is dedicated to bridging the gap between complex legal principles and everyday understanding by delivering accurate, practical, and accessible legal information. His vision is to promote a legally informed society where individuals, businesses, and communities can confidently understand their rights, responsibilities, and available legal solutions. Through LegalJamii, he continues to advance legal literacy by transforming legal concepts into clear and simplified language for the benefit of the wider public.

Leave a Reply

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Discover more from ๐‹๐„๐†๐€๐‹๐‰๐€๐Œ๐ˆ๐ˆโš–๏ธ

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading